Tuesday, May 29, 2012







VYAMA vya upinzani wilaya ya Ludewa na mkoa wa Iringa vimeungana na wapiga kura wa jimbo la Ludewa mkoa mpya wa mkoani Njombe kufanya mapokezi makubwa ya kihistoria kwa mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe (CCM) wananchi na vyama vya upinzini katika jimbo hilo wakitoa msimamo mzito kwa chama cha mapinduzi (CCM) kuwa iwapo kitajaribu kumfanyia mizengwe mbunge huyo kwa hatua yake ya aliyoifanya mbunge Dodoma kwa kusaini fomu ya kutokuwa na imani ya waziri mkuu Mizengo Pinda basi jimbo watalikosa.

Wapiga kura hao wa jimbo la Ludewa ambao waliungana na vyama vya TLP ,CUF,NCCR Mageuzi pamoja na wana CCM katika mandamano makubwa yaliyoanzia umbali wa zaidi ya kilometa 10 hadi mjini Ludewa huku mbunge Filikunjombe akitumia usafiri wa punda ,walitoa kauli hiyo leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya michezo vya Ludewa mjini.

Akizungumza kwa niaba ya vyama vya upinzani katika mkutano huo katibu mwenezi wa TLP mkoa wa Iringa Branka Haule alisema kuwa uamuzi wa mbunge huyo Filikunjombe wa kuweka sahihi katka fomu iliyoandaliwa na mbunge Zitto Kabwe (Chadema) kuhusiana na kutokuwa na imani ya waziri mkuu kutokana na baadhi ya mawaziri wake kufanya ufisadi wa kutisha ,ni uamuzi uliopokelewa kwa furaha kubwa na watanzania wote pasipo kujali itikadi zao za kisiasa .

Hivyo alisema wao kama vyama vya upinzani wanaungana na hatua ya mbunge Filikunjombe na wabunge wote waliopinga vitendo vya ufisadi na utendaji mbovu wa mawaziri waliotemwa katika baraza jipya lililoundwa baada ya wabunge kutangaza kutokuwa na imani na waziri mkuu Pinda .

Haule alisema wao kama TLP na vyama vyote vya upinzani ambavyo vinapinga vitendo vya ufisadi wataendelea kutoa ushirikiano kwa mbunge Filikunjombe katika jimbo hilo la Ludewa na kutokana na hatua ya mbunge huyo kuonyesha uzalendo kwa umma bila kuangalia chama chake cha CCM wao wataendelea kumuunga mkono hata katika uchaguzi mkuu ujao na iwapo CCM itajaribu kumfanyia fitina basi watakuwa tayari kumuunga mkono popote atakapo kwenda .

Viongozi wa upinzani walioshiriki maandamano hayo ni mbali ya Haule ni pamoja na kampeni meneja mkuu wa mkoa kupitia TLP mkoa wa Iringa Mrisho Samson , mwenyekiti wa NCCR Mageuzi wilaya ya Ludewa ,Lazaro Mwinuka , Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Ludewa Asungushe Mtweve, Katibu mwenezi wa TLP wilaya , Bariki Pangisa , katibu wa wilaya ya Ludewa TLP ,Joseph Kayombo na katibu wa CUF wilaya ya Ludewa Edwin Mgimba huku viongozi wa Chadema wilaya hiyo wakishiriki wakiungana na wananchi katika mkutano na kugoma kutambulishwa .

Kwa upande wa CCM walioshiriki ni pamoja na makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Ludewa Monica Mchilo, katibu mwenezi wa CCM mkoa Mgaya pamoja na mwenyekiti wa CCM wilaya na madiwani .

Kwa upande wao wananchi wa jimbo la Ludewa katika risala yao iliyosomwa na Casta Mbawala walisema kuwa wataendelea kumuunga mkono mbunge huyo popote atakapokuwa akitetea maendeleo ya Taifa bila kujali itikadi zao za kisiasa .

Akiwahotubia wananchi hao mbunge Filikunjombe mbali ya kuwapongeza kwa mapokezi makubwa aliyopata bado alisema kuwa ataendelea kupigania maendeleo ya wilaya ya Ludewa na Taifa kwa ujumla .

Alisema kuwa mjadala katika Bunge liliopita juu ya ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na taarifa za mwaka za Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma unaonyesha ni namna gani vitendo vya kifisadi vya viongozi wetu waandamizi vinazuia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010 kama tulivyoahidi kwa watanzania.

“Ndugu wananchi wenzangu, nikiwa mle bungeni, tukiwa tunaijadili ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, inayoonyesha ubadhirifu mkubwa katika fedha za umma; ghafla mawazo yangu yalihama kutoka bungeni yakaja katika vijiji vyetu vya Ludewa, Mavanga, Lusala, Lumbila, na kadhalika. Kitu kama mshale wenye ncha kali wa moto uliuchoma moyo wangu.”

Filikunjombe
alisema kuwa alikumbuka mateso makubwa wanayopata wananchi wake na ndio sababu akaumia sana .

“Wakati baadhi ya Mawaziri, wanatumia nafasi zao kujineemesha, nilikumbuka jinsi mwananchi wa Ludewa anavyotaabika kwa miundombinu duni. …Nilikumbuka jinsi tulivyo na bara bara mbovu. Nilikumbuka jinsi mwananchi wa Ludewa anavyocheleweshewa kuletewa Pembejeo za Kilimo. Nilikumbuka jinsi mwananchi wa Ludewa anavyoletewa mbegu za kupandia mwezi wa pili wakati msimu wa kupanda mahindi ni mwezi Novemba”alisema

“Nilikumbuka Jinsi mawakala wa Pembejeo wanavyokopwa mbolea na serikali yetu, na hakuna kauli maalum inayotolewa. Nikaumia sana…. Nilikumbuka namna wanafunzi wa Ludewa wanavyosoma katika mazingira duni, wamekaa chini, walimu hawatoshi, madarasa hayatoshi, nyumba za walimu hazitoshi. Nilikumbuka namna sekondari zetu zinavyokosa maabara. Nilizidi kuumia moyoni mwangu.”
“Kwa niaba yenu ninafarijika kwamba Mhe. Rais ameshaanza kuchukua hatua za kuwawajibisha wahusika. Wito wangu kwake Mheshimiwa Rais ni kwamba asiishie tu kuwawajibisha tu wahusika bali ni lazima pia wafikishwe mahakamani ikiwa ni pamoja na kufilisiwa mali zao walizozipata kwa njia ya kifisadi.”
Alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi kinachafuka kwa sababu tu ya kuwakumbatia watu wachache wanaofanya wasiowaaminifu na mafisadi ambao sio Sera ya CCM na wala siyo malengo wala madhumuni kwa mujibu wa Katiba ya chama chetu.
“Vita tuliyoianzisha ya kukomesha ubadhilifu, wizi, matumizi mabaya ya madaraka na rushwa ni vita takatifu ambayo kila mmoja wetu anatakiwa kushiriki kwa eneo lake, silaha yetu kubwa ikiwa ni ukweli, haki na ujasiri. Kamwe, msidhani sisi tuliosimama mle bungeni kuwasema wale mawaziri wetu kwamba tunawachukia. Hapana. Bali ukweli ni kwamba kwenye hili ninawapenda zaidi wana Ludewa, na tunalipenda sana Taifa letu kuliko tunavyowapenda wao”.

Na McDonald Mollel Masse-Ludewa


 

No comments:

Post a Comment