Moto ukiwaka katikati ya mtaa mjini Zanzibar jana baada ya vurugu za wanaharakati kupinga muungano na kudai Zanzibar ijitawale.
ZANZIBAR imechafuka. Baada ya kuwapo kwa amani kwa takribani mwaka mmoja
tangu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, vurugu na hali
ya wasiwasi zimeibuka tena baada ya wanaharakati wa Kiislam kufanya
maandamano kutaka uhuru wa visiwa hivyo.
Zanzibar ilijikuta katika
hali tete kiusalama tangu mwaka 1995 baadaya kutangazwa matokeo ya
uchaguzi mkuu wa Rais, ambayo Chama cha Mapinduzi (CCM) kiilibuka
kidedea na Chama cha Wananchi (CUF) kupinga, lakini uhasama huo ulizikwa
Julai 31 mwaka 2010, baada ya kura ya maoni ya kuunda Serikali hiyo ya
umoja wa kitaifa.
Lakini kuanzia juzi usiku hadi jana jioni mji
wa Unguja na viunga vyake ulitikiswa na mabomu ya kutoa machozi ambayo
polisi waliyatumia kutawanya mamia ya wanaharakati hao wa Kiislam
wakiongozwa na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar
(JUMIKI).
Mabomu ya machozi yalipigwa mfululizo juzi usiku na
kuendelea kutwa nzima jana, hivyo kuathiri shughuli za biashara, ibada
katika makanisa mbalimbali na kusababisha hofu kwa wananchi.
Kwa
muda wa saa takriban mbili hivi kati ya saa 3:00 na saa 5:00 asubuhi,
helkopta ya polisi ilikuwa ikipasua anga la Zanzibar ambalo lilikuwa
limetandwa na moshi uliotokana na mabomu ya machozi pia uchomaji wa
matairi ya magari.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa
Ali Mussa aliwaambia waandishi wa habari kuwa wafuasi hao wamefanya
uharibifu mkubwa ikiwa pamoja na kuchoma moto makanisa mawili na kwamba,
watu saba akiwamo Imamu wa Msikiti wa Bizeredi, Maalim Mussa Juma
wanaotuhumiwa na matukio hayo wamekamatwa na jeshi hilo.
Akizungumza
na Mwandishi wa habari hizi Kiongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies
of God (TAG), Askofu Dickoson Maganga alisema watu wasiojulikana
walivamia kanisa lao eneo la Kariakoo Mjini Zanzibar mnamo saa 4.30
usiku na kuvunja ukuta, kuchoma viti vya plasitiki pamoja na gari yake.
Chanzo
cha vurugu hizo kinatajwa kuwa ni wanaharakati hao juzi kufanya
mkusanyiko na maandamano makubwa ya kushtukiza ambayo yalizistua mamlaka
za usalama visiwani humo, lakini baada ya kutawanyika jioni baadhi ya
viongozi wa maandamano hayo walitiwa mbaroni.
Baada ya kukamatwa
kwao, wafuasi wao walikusanyika makao makuu ya polisi Mkoa wa Mjini
Magharibi, Madema, kushinikiza kutolewa kwa viongozi hao wanaoshikiliwa
kituoni hapo.
Habari zaidi zinasema kutokana na hali ilivyo,
askari polisi walitarajiwa kuongezwa visiwani humo, ili kusaidia
kuimarisha hali ya usalama pia kuwadhibiti wahalifu ambao walikuwa
wameanza kuelekea nje ya maeneo ya mji.
Tayari kuna taarifa kuwa
askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutoka
Tanzania bara jana mchana walingia Zanzibar kwa ajili ya kuongeza ulizi
katika mji wa Unguja.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza
hakuna kiongozi yoyote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)
aliyetoa kauli kuhusu hali hiyo.
Kauli ya PolisiKamishna
Mussa alisema jeshi lake litaendelea kuwasaka na kuwatia mikononi wote
waliopanga fujo hizo pamoja na viongozi wote wa JUMIKI.
“Jumuiya
ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar ndio iliyohusika na
kuwachochea vijana kukusanyika na kufanya uharibifu ikiwemo kuchoma moto
gari, kupanga mawe barabarani na kufanya hujuma mbalimbali kinyume cha
sheria. Tutaendelea kuwasaka kwa gharama zote,” aliapa Kamishna Mussa.
Alifafanua
kwamba kwa sasa mikusanyiko yote ya mihadhara ya kidini na vyama vya
siasa, lazima ipate kibali cha polisi vyinginevyo jeshi lake litatumia
nguvu za ziada kutawanya mikusanyiko hiyo ili kulinda sheria za nchi,
amani na utulivu.
Hata hivyo, kamishna huyo wa polisi alijizuia
kuhusisha harakati za Uamsho na chama cha siasa wala kutaja majina ya
viongozi ambao tayari wanashikiliwa na jeshi lake.
“Mpaka sasa
hivi sina majina yao kwa jumla, lakini tumewakamata viongozi wa Uamsho
na tunatendelea kuwasaka lakini jina moja tu ndio ninalo ambalo ni Mussa
Abdallah Juma,” alisema Kamishna huyo.
Hali bado teteWakati
jeshi la polisi litoa onyo hilo, hali ya usalama ilionekana kuwa bado
tete huku maeneo kadhaa ya Mji wa Zanzibar hasa Darajani na Michenzani
ambako muda wote ni sehemu zenye harakati nyingi za biashara, jana
zilikuwa zimebakia bila pilikapilika kutokana na askari waliojihami
kufanya doria katika mitaa yote na kulipua mabomu kila penye kikundi cha
watu waliokusanyika wakinywa kahawa.
Mitaa hiyo ilikuwa
imechafuliwa kwa mawe, matofali na magogo yaliowekwa barabarani ili
kuziba njia kwa ajili kuzuia magari yasipite huku mipira ya magari
ikiwashwa moto na vijana hao.
Kwa upande wake Askofu Maganga akizungumzia uvamizi kisha uhalifu uliofanywa kanisani kwake alisema:
“Nasikitika
sana kwa tukio hili ambalo tayari tumeiarifu polisi ambao jana (juzi),
usiku walifika hapa wakishirikiana na kikosi cha kuzima moto na
kufanikiwa kuuzima moto huo ambao kwa habati nzuri haujaathiri paa la
kanisa letu,” alishukuru kiongozi huyo.
Alisema kundi la watu
ambalo lilikuwa likitoa maneno ya kashfa na kutishia maisha ya waumini
waliokuwa wakifanya ibada usiku huo, lilikatisha ibada hiyo pamoja na
kusababisha uharibifu wa mali ya kanisa hilo yenye thamani ya zaidi ya
Sh 100 millioni.
Kauli ya JUMIKIKutokana na
hali hiyo, jumuiya hiyo jana ilitoa taarifa yake kwa vyombo vya habari
ikikanusha kuhusika na kuchochea watu kuchoma kanisa wala kuharibu mali
za watu.
Hata hivyo, Katibu wa Jumuiya hiyo, Abdallah Said
alisema katika taarifa hiyo kwamba jeshi la polisi linapaswa kubeba
lawama kwa yote yaliotokea kutokana na kuvunja sheria na kuwakamata
viongozi bila ya utaratibu wa busara.
“Uislamu ni dini ya amani
na inahimiza ushirikiano na utulivu na hatuwezi kuwatuma watu kwenda
kuvunja makanisa na kuharibu mali, kwa sababu ndani ya imani zetu
tunajua hilo ni kosa na jambo ambalo halifai katika maamrisho ya dini
yetu,” alisema Sheikh Abdallah.
Taarifa hiyo ilisema pia kwamba
jumuiya hiyo imekuwa wazi katika kudai maslahi ya Zanzibar na sio
vinginevyo na kuahidi kufanya hivyo kwa njia za amani, na iwapo watakuwa
wamekosea basi wapo tayari kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Ni
lazima polisi wajue kwamba tupo tayari kufanya kazi kwa misingi ya
kisheria na hata kwa kujisalimisha tupo tayari, lakini ukamataji bila
kufuata busara na sheria haukubaliki. Tunachokitaka ni kura ya maoni
haraka na hilo tutaendelea kulidai,” alisisitiza katibu huyo wa JUMIKI.
Wakati
viongozi wa Uamsho wakiendelea kutafutwa na jeshi la polisi, nyumba ya
kiongozi aliyeongoza maandamano juzi Sheikh Farid Hadi Ahmed inadaiwa
kuvunjwa milango usiku wa manane alipokuwa akiswakwa jeshi hilo.
Hata
hivyo, taarifa hizo hazikuthibitishwa iwapo ni polisi waliofanya
kitendo hicho au la, wanafamilia wanasema waligongewa milango na
kutakiwa wafungue baada ya kutofungua walisikia kishindo kikubwa cha
kusukumwa milango katika eneo la Mbuyuni Mjini Unguja.
Vijana
katika mitaa ya Zanzibar jana walionekana wakiwa na hamasa kubwa wakidai
kuendelea kuungana na viongozi wao kudai haki ya Zanzibar, pamoja na
kutaka Zanzibar huru kutoka ndani ya mikono ya Muungano.
“Sisi
tunachokitaka Zanzibar yetu watupige mabomu, watuue, watukamate lakini
tunataka Zanzibar yetu na hatusikii lolote,” walisikika baadhi ya
vijana.
Hada jana jioni vurugu katika badhi ya maeneo hususan
Kwelekwe na njia ya Baa ya Amani zilikuwa zikiendelea na gari moja
lilichomwa moto karibu na ofisi ya CCM.
Matukio kablaZanzibar
imekuwa ikitawaliwa na matukio ya ghasia ambayo licha ya mihadhara hiyo
ya Kiislam ilikuwa ni uhasama wa kisiasa kati ya vyama vikuu vya CUF na
CCM, hatua ambayo iliwahi kusababisha mauaji ya Januari 27, mwaka 2001.
Lakini,
uhasama huo wa kisiasa ambao ni wa kihistoria ulizikwa baada ya kura
hiyo ya maoni na uchaguzi mkuu wa 2010 hatua ambayo imemfanya Katibu
Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa
SMZ huku baadhi ya mawaziri pia wakitoka katika chama hicho.
Hata
hivyo, wanaharakati hao wa Kiislam wameanza upya kuilipua Zanzibar
wakishinikiza visiwa hivyo viwe taifa huru kwa kujitenga katika Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Zitto ataka tume ya uchunguziKatika
hatua nyingine Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amemtaka Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aunde kikosi kazi maalum kwa ajili ya
kudhibiti
vurugu hizo na kuanza mazungumzo na pande zote kwa kuwa, "Hiki sio kitendo cha kudharau
kabisa."
Alifafanua kwamba waliochoma nyumba za ibada wasakwe na kufikishwa mbele ya sheria mara
moja na kuongeza, "Tusiruhusu hata kidogo wapuuzi wachache kutuingiza katika vurugu za
kidini ili kufikia malengo yao ya kisiasa."
mwisho